Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
MSHAMBULIAJI wa Chipukizi, Faki Mwalim ndiye anayeongoza kwa mabao kwa kupachika wavuni mabao matano mpaka sasa, katika Ligi Kuu ya Grand Malt inayoendelea.
Timu zote mpaka sasa zimeshuka uwanjani mara tano, huku Bandari ikiwa inaongoza ligi hiyo kwa kujikusanyia pointi 13, huku Falcon ikiburuza mkia ikiwa na pointi moja tu.
Wakati Faki akiongoza kwa mabao hayo, anafuatiwa kwa karibu na Ali Manzo Mnyovela wa Mtende mwenye mabao manne, huku waliofunga matatu wakiwa ni Mohd Abdurahim wa Mtende na Amour Suleiman anayekipiga Malindi.
Wengine na timu wanazotoka kwenye mabano ni Mussa Omar (Malindi), Mfaume Shaaban (Jamhuri) na Jaku Joma Jaku (Mafunzo), huku aliyepachika mawili akiwa Haitham Khamis (Bandari).
Pamoja na Bandari kuongoza ligi hiyo kwa kujikusanyia pointi hizo, inafuatiwa kwa karibu zaidi na Mtende yenye pointi 10.
Duma ndio yenye kadi nyingi za njano, ikiwa mpaka sasa wachezaji wake wameonyeshwa kadi hizo mara 12, ikiwa pia na kadi moja nyekundu. Mafunzo na Zimamoto kila moja ina kadi mbili nyekundu.
Ligi Kuu ya Grand Malt inatarajiwa kuendelea tena leo kwa mchezo mmoja, wakati Mafunzo itakapoikaribisha Chuoni katika Uwanja wa Amaan, wakati kesho Mtende itakuwa na kibarua kizito kwa KMKM katika uwanja huo.
Jumamosi Malindi itaivaa Chikupikizi ndani ya Uwanja wa Amaan, huku kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba kukiwa na pambano kati ya Duma na Mundu na siku inayofuata Mafunzo ikiivaa Jamhuri ndani ya Amaan.
Ligi Kuu ya Zanzibar ambayo kwa sasa inajulikana kama Grand Malt Premier League inadhaminiwa na kinywaji cha Grand Malt kisicho na kilevi.
No comments:
Post a Comment