Tangazo

March 14, 2013

Tanzania kujikita kwenye nishati jotoardhi

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele (pichani), amewataka wataalamu kuharakisha mchakato wa upatikanaji nishati ya jotoardhi (geothermal), ili kukabiliana na upungufu wa tatizo hilo.

Akifungua warsha ya sheria na kanuni za jotoardhi Dar es Salaam jana, Waziri Masele alisema matumizi ya umeme nchini yanaongezeka kwa kasi.

“Kutokana na kuongezeka kwa uwekezaji, ongezeko la watu na fursa, mpango wa matumizi ya umeme unaonyesha watumiaji wataongezeka kutoka asilimia 18.4 hadi asilimia 75 ifikapo mwaka 2035,” alisema Masele na kuongeza:

“…mkakati uliopo ni kujikita kwenye nishati endelevu hasa jotoardhi.”
Kuhusu mikakati ya Serikali, Masele alisema Sera ya Nishati ya mwaka 2003 inaruhusu matumizi ya vyanzo vya nishati vya kienyeji ili kukidhi mahitaji ya Taifa.

Alizitaja sehemu ambazo Serikali imeainisha kuwa ni vyanzo vya jotoardhi, ambavyo vina uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 650 na viko kwenye ukanda wa Bonde la Ufa Afrika Mashariki.

“Vipimo vinaonyesha kuwapo kwa joto kali Ziwa Manyara, Natron, Kreta ya Ngorongoro na Songwe Mbeya, huku joto la chini limejionyesha Ziwa Eyasi na eneo la Majimoto, Musoma,” alisema Masele.

Aliongeza kuwa utafiti zaidi unaendelea hasa maeneo ya milima ya volkano ya Rungwe mkoani Mbeya, Ngorongoro na Manyara zinazoonyesha kuwapo kwa jotoardhi kubwa kuliko maeneo mengine.

“Tafiti zaidi zinaonyesha eneo la Mbeya hasa Songwe kama eneo muhimu la kupata nishati hiyo. Utafutaji wa jotoardhi Ziwa Ngozi la Songwe umekuwapo tangu mwaka 2006 hadi leo ukihusisha Wizara ya Nishati na Madini,” alisema Masele.

Naye Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB),
Tonia Kandiero alisema benki hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za upatikanaji nishati endelevu kwa nchi za Afrika.

Balozi wa Uingereza nchini, Dianna Melrose alisema wataendelea kuisaidia Tanzania. kutafuta nishati endelevu ili kukuza maendeleo ya uchumi na jamii.

Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felichism Mramba alisema mikakati hiyo haitatatua tatizo la sasa la upungufu wa umeme, bali ni mipango ya baadaye.

No comments: