Tangazo

March 7, 2013

Wananchi kuanza kuomba Ujumbe Mabaraza ya Katiba Kesho Ijumaa

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba akiongea katika mkutano na wanahabari leo katika ofisi za Tume jijini Dar es Salaam. Kulia ni Katibu wa Tume Bw. Assaa Rashid.
Na Mwandishi Wetu

Wananchi wenye sifa za kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na ambao wangependa kuwa Wajumbe wa Mabaraza wanaweza kuanza kuwasilisha maombi yao kwa Maofisa Watendaji wa Vijiji au Mtaa kuanzia kesho (Ijumaa, tarehe 8 Machi, 2013) hadi tarehe 20 Machi mwaka huu (2013). Kwa Zanzibar, maombi hayo yawasilishwe kwa Masheha.

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba amesema jijini Dar es Salaam leo (Alhamisi, Machi 7) kuwa ili kuhakikisha mchakato wa uundwaji na uendeshaji wa Mabaraza ya Katiba unaendeshwa kwa ufanisi, Tume imeandaa Mwongozo wa kusimamia mchakato huo na kuuchapisha katika magazeti mbalimbali na kuwekwa katika tovuti ya Tume (www.katiba.go.tz) na ukurasa wa facebook wa Tume (tumeyamabadilikoyakatiba).

Jaji Warioba ameongeza kuwa Tume yake pia imechapisha vitabu vyenye mwongozo huu na kuvisambaza kwa Ofisi za Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Miji, Manispaa, Majiji na wadau wengine kwa Tanzania Bara ili wawafikishie wananchi katika mitaa na vijiji. Kwa Zanzibar, mwongozo umesambazwa kwa Ofisi za Wakuu wa Wilaya, Baraza la Manispaa na Katibu wa Halmashauri za Mji ili wawafikishie wananchi katika Shehia zao.

“Sifa za mwananchi anayependa kuomba nafasi ya kuwa mjumbe wa Baraza la Katiba ni pamoja na kuwa raia wa Tanzania na awe na umri wa miaka 18 au zaidi,” amesema Jaji Warioba katika mkutano wake na wanahabari uliofanyika katika ofisi za Tume.

Jaji Warioba alitaja sifa nyingine kuwa ni pamoja na kuwa na uwezo wa kusoma na kuandika na pia awe ni mkazi wa kudumu wa Kijiji, Mtaa au Shehia husika. Sifa nyingine ni pamoja na kuwa mtu mwenye hekima, busara na uadilifu na ambaye ana uwezo wa kujieleza na kupambanua mambo.

Katika mwongozo huo, Jaji Warioba amesema, Tume pia imeelekeza kuwa wananchi wanaoomba wanapaswa kuwasilisha nakala mbili za barua ya maombi. Barua moja itabaki katika Ofisi ya Mtendaji na barua ya pili atabaki nayo mwombaji baada ya kutiwa saini na kugongwa muhuri kuthibitisha kuwa ombi lake limepokelewa.

Aidha, baada ya muda wa kuwasilisha maombi kukamilika, Tume imeelekeza katika mwongozo wake kuwa majina ya waombaji wote yatapaswa kuwa katika sehemu za wazi na mbao za matangazo za ofisi za Watendaji wa mitaa au vijiji kuanzia tarehe 22 – 28 Machi mwaka huu ili wananchi waweze kuyapitia na kujiridhisha kuwa maombi yao yamepokelewa.

Mwongozo wa Tume pia umeelekeza kuwa kuanzia tarehe 30 Machi hadi 3 Aprili kutafanyika Mikutano Mikuu Maalum ya Mitaa, Vijiji au Shehia kwa Zanzibar ili kufanya uchaguzi na kufuatiwa na Vikao Maalum ya Maendeleo vya Kata vitakayofanyika kati ya tarehe 5 hadi 9 Aprili mwaka huu ili kuchagua wawakilishi wa kila wa Kata.

Majina hayo yatawasilishwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji, Manispaa au Jiji kwa Tanzania Bara na Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa, Katibu wa Halmashauri Mji/ Wilaya kwa Zanzibar ambao watayawasilisha kwa Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa uteuzi rasmi.

Jaji Warioba amewaomba wananchi na viongozi wote kuendesha mikutano ya uundwaji wa mabaraza kwa amani na utulivu na kuzingatia mwongozo uliotolewa na Tume.

No comments: