Tangazo

March 7, 2013

Kuongezeka kwa joto, kupotea kwa baadhi ya viumbe baharini na kumezwa kwa visiwa ni miongoni mwa athari za mabadiliko ya Tabianchi

Na Evelyn Mkokoi
 
Bagamoyo
Kuongezeka kwa joto katika pwani ya Tanzania, kupotea kwa baadhi ya viumbe katika bahari na hindi na kumezwa kwa visiwa kumeelezwa kuwa ni miongoni mwa athari zitokanazo mabadiliko ya tabia nchi.
 
Hayo yameelezwa leo na Naibu Katibu Mkuu katika Ofisi ya Makamu wa Rais Injinia Ngosi Mwihava (pichani), katika warsha ya wadau ya programu ya kitaifa ya kuhimili athari zitokanazo na madhara ya mabadiliko ya tabia nchi katika ukanda wa pwani inayoendelea mjini Bagamoyo.

Injinia Mwihava ameeleza kuwa, athari nyingine zitokanazo na  madhara hayo ni pamoja na visiwa baridi kuingiliwa na maji ya chumvi, vina vya bahari kuongezeka na kwa kuwa viumbe katika bahari hupotea inaweza kupelekea uchumi wa wakazi wengi wa mwambao kudidimia kwani hutegemea zaidi uvuvi.

Tanzania kama nchi “Ina mkakati wa kuongeza uelewa kwa kushirikiana na wadau juu ya dhana ya namna ya kukabiliana na madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi kwa kushirikiana na wadau na wananchi wa kawaida kwa kutumia sayansi na elimu asilia ikiwa ni pamoja na kufuga samaki iliwaweze kusaidiaa kipindi ambacho watakuwa wamepotea.

Kwa upande wake mkurugenzi wa mradi wa pwani bwana Baraka kalangale ameeleza kuwa ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi mradi wake unawajengea uwezo  wananchi katika eneo hilo kupitia mafunzo na ushirikishwaji.

“Vijiji vingi vimeathirika na masuala haya ya mabadiliko ya tabia nchi ikiwa ni pamoja na kijiji cha mbuyuni katika wilaya ya pwani kwani kipo katika hatari ya kumong’onyoka kabisa, alisisitiza.”

Warsha hiyo inayohusisha wadau kutoka mashirika mbali mbali yanayojihusisha na masuala ya mazingira na serikali kuu imefadhiliwa na shirika la misaada la watu wa marekani (USAID).

No comments: