Tangazo

March 11, 2013

Wanawake Wajasiriamali watakiwa kutengeneza bidhaa bora

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete
Na Anna Nkinda – Magu

Kina mama Wajasiliamali nchini wametakiwa kuongeza ubunifu katika vikundi vyao ikiwa ni pamoja na kutengeneza bidhaa  bora zaidi ambazo  zitakidhi kiwango cha kimataifa na hivyo kuwa na soko la uhakika la ndani na nje ya nchi.

Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wanawake wajasiliamali wa mkoa wa Mwanza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya mwanamke Duniani zilizofanyika katika kituo cha utamaduni Bujora wilayani Magu.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) pia aliwataka wanawake hao  wajasiriamali kutengeneza mazingira mazuri ya kufanyia kazi na  kutafuta masoko ya bidhaa zao hasa mayai na vyakula ambayo yanapatikana kirahisi katika mkoa wa Mwanza na mikoa jirani.

Aliendelea kusema kuwa hivi sasa kina mama wengi wanaungana na kufanya kazi kwa pamoja katika vikundi vya ujasiriamali  hii ni ishara kuwa kila mwanamke anashauku ya kufanya kazi ya maendeleo bila ya kutegemea msaada wa mwanaume.

Mama Kikwete alisema, “Ninawashukuru kwa kazi njema mnazozifanya na ninapenda kuwahakikishia kuwa niko nanyi katika mihangaiko na juhudii zenu zote. Nitajitahidi niwezavyo na kadri Mungu atakavyonijalia kuwawezesha katika elimu ya ujasiriamali kupitia taasisi ya WAMA kila itakapowezekana”.

Mwenyekiti huyo wa WAMA alisisitiza kuwa juhudi za ukombozi wa mwanamke zilianza zamani na mtu mmojammoja. Lakini kwa sasa juhudi hizi zinapaswa kuenziwa  kwa mshikamo na kuwa wamoja zaidi ili kila mtu kwa nafasi yake aweze  kumkomboa mwanamke kielimu na kiuchumi.

Akisoma taarifa ya wanawake wajasiliamali hao Mwadawa Tofiki alisema kuwa wanajishughulisha na usindikaji wa vyakula, upambaji, upishi, ufugaji, ufumaji, utegenezaji wa sabuni na batiki, ufinyanzi, uhunzi, vikoba, uwekaji wa hisa, Vyama vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS),sanaa na burudani.

“Licha ya kujishughulisha na kazi za ujasiliamali pia tunatoa huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, yatima na wenye maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) , wajane, wazee na watu wenye ulemavu.

Kauli mbiu ya mwaka 2013 ni “Uelewa wa masuala ya jinsia katika jamii ongeza kasi”, ambayo inaonyesha wazi kwamba sisi wanawake tunayo majukumu makubwa na muhimu kifamilia na kijamii kama vile kulea na kushirikiana na wanaume katika shughuli za kijamii na uzalishaji mali” alisema Tofiki.

Alizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni  elimu duni katika masuala ya ujasiliamali na sheria, ushirikishwaji duni katika masuala ya kkijamii, kiuchumi na kisiasa, huduma duni ya afya ya mama na mtoto, baadhi ya kina baba kutelekeza familia zao, wanawake kunyimwa haki ya kulimiliki au kurithi mali.

Ukosefu wa masoko kwa bidhaa za uzalishaji mali kama vile kilimo cha mbogamboga , ufugaji na usindikaji wa vyakula na matunda, gharama kubwa za upatikanaji wa pembejeo, wajane na watoto yatima kutokupewa kipaumbele katika utoaji wa huduma za afya na uporomokaji wa maadili katika jamii.

Taasisi ya WAMA iliwachangia wanawake hao wajasiliamali  shilingi milioni tano fedha ambazo watagawana katika vikundi vyao na ziwatasaidia kuinua mitaji yao  ili waweze kuwa endelevu katika shughuli zao za maendeleo.

No comments: