Tangazo

October 17, 2013

Mama Kikwete awataka wanawake mkoani Iringa kuachana na tabia ya kujifungulia majumbani

Na Anna Nkinda- Maelezo, Iringa

Wanawake mkoani Iringa wametakiwa kuitumia Hospitali ya rufaa ya mkoa huo kupata huduma ya uzazi pamoja na watoto wao na  kuachana na  tabia ya kujifungulia majumbani, kupeleka watoto kwa waganga wa jadi kwa kudhani kuwa magonjwa wanayoumwa hayawezi kutibika Hospitalini.

Wito huo umetolewa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete (pichani), wakati akifungua jengo la huduma za watoto katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa ambayo imejengwa kwa msaada wa Hospitali rafiki ya Vicenza iliyopo katika mkoa wa Veneto nchini Italia.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuna baadhi ya wazazi  wakiona watoto afya za watoto wao zinadhoofika   ikiwa ni pamoja na kuumwa ugonjwa wa utapiamlo wanadhani kuwa jirani zao wanawaonea wivu na kuwaroga  na wanaona njia sahihi ni   kwenda kwa waganga wa jadi badala ya kuwapeleka Hospitali ili  wakaonane na wataalamu wa afya.

Alisema vifo vya watoto wadogo wenye umri wa chini ya miaka mitano kwa sasa ni 54 katika kila watoto wanaozaliwa wakiwa hai 1000 na katika mkoa huo idadi ya vifo hivyo ni watoto 20 kwa kila vizazi hai 1000 nia ya Serikali ni kuhakikisha kuwa vifo hivyo vinapungua ili kuweza kufikia malengo ya Maendeleo ya Milinia ifikapo mwaka 2015.

Aidha Mama Kikwete pia aliwataka wakazi wa mkoa huo kujiepusha na mazingira yawatayowapeleka kupata maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi na kuwa waaminifu katika ndoa zao na kwa wale ambao hawana ndoa watulie na kujitunza huku wasubiri muda wao wa kuoa au kuolewa ukifika.

“Mkoa huu maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) yako juu takwimu zinaonyesha kuwa watu tisa kati ya 100 wanamaambukizi , hivyo basi nawasihi mjitunze na kuheshimu ndoa zenu kwa kufanya hivyo hamtaweza kupata maambukizi ya ugonjwa huu kirahisi ingawa unaweza ukapata kwa njia nyingi lakini maambukizi mengi yanapatikana kwa njia ya kufanya mapenzi yasiyo salama”, alisema Mama Kikwete.

Mkuu wa mkoa wa Iringa  Dkt. Christine Ishengoma aliushukuru uongozi wa mkoa wa Veneto na Hospitali ya Vicenza kwa msaada wa ujenzi wa wodi ya watoto na ujenzi wa jengo la kujifungulia kina mama wajawazito.

Dkt. Ishengoma aliahidi atahakikisha na kusimamia ili  jengo hilo liweze kutumika  kama lilivyokusudiwa na wahudumu wa Hospitali hiyo waweze kutoa huduma bora kwa wananchi wa mkoa wa Iringa. 

Akisoma taarifa ya ujenzi wa jengo hilo mganga mkuu wa mkoa Dkt. Robert Salim alisema jengo hilo ni awamu ya pili ya ujenzi kwani awamu ya kwanza ilikuwa ni ujenzi wa jengo la kujifungulia wajawazito ambalo kwa kiasi kikubwa limeboresha huduma na kupuza vifo vya wazazi na watoto wachanga.

Dkt. Salim  alisema lengo la kujengwa kwa wodi ya watoto ni kuboresha huduma ya afya, kupunguza vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano vinavyotokana na magonjwa ya kuambukiza na kupunguza msongamano katika wodi ya watoto.

"Faida za mradi huu ni kuboresha utoaji wa huduma kwa urahisi kwa watoto wagonjwa kwa kuwa na eneo kubwa la kufanyia kazi, kupunguza  msongamano na kutatua tatizo la wagonjwa kulala wawili wawili au zaidi katika kitanda kimoja.

Pia ni kupunguza maambukizi ya magonjwa kwa watoto waliolazwa , kuwa na eneo la kutolea elimu ya lishe kwa watoto na kuwapatia watoto eneo la michezo na kupenda kusoma", alisema Dkt. Salim.

Kwa upande wake Balozi wa Italia nchini Luigi Scotto aliwashukuru watu wote waliohusika hadi kukamilika kwa mradi huo na kusema   anajivunia kuwa balozi katika nchi ya Tanzania yenye ambayo watu wake ni wakarimu na wenye ushirikiano wa hali ya juu.

Kukamilika kwa mradi huu ambao ni moja ya kazi zinazofanywa na n chi ya Itali hapa Tanzania inaonyesha mahusiano mazuri ya kirafiki ambayo yalikuwepo kwa muda mrefu kati ya nchi hizi mbili nitaendelea kuhakikisha kuwa tunaimarisha sekta ya afya hapa nchini ili watanzania wapate huduma bora”, alisema Balozi Scotto.

Naye Katibu Tawala (RAS) wa mkoa wa Veneto nchini Italia Roberto Ciambetti alisema uhusiano kati ya hospitali ya Vicenta ya nchini humo  na Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa mwaka 2003 ukiwa ni muendelezo wa miradi iliyoanzishwa  na shirika lisilo la kiserikali la  “Doctor with Africa CUAMM” la nchini humo.

Alisema shirika la Doctor with Africa CUAMM linafanya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuandaa na kutengeneza miradi ya afya ya ushirikiano, kuwaleta madaktari bingwa na wataalamu wengine wa afya katika nchi za Afrika, kuwasomesha madaktari katika fani za afya, kufanya tafiti za afya na kutekeleza program za uelimishaji jamii.

Alisema Hospitali ya Vicenza imekamilisa miradi miwili na a Hospitali ya rufaa ya Iringa ambayo malengo yake ni kutoa msaada wa kitaaluma  ili kuboresha ubora wa huduma, kuanzisha progeamu ya kubadilishana wataalamu kati ya pande mbili ili kuboresha zinazotolewa.

Kuisaidia Hospitali ya Rufaa ya mkoa kupata vifaa vya kisasa na vifaa tiba, kuwasomesha watumishi wa hospitalikwenye fani mbalimbali ndani nan je ya nchi na kuboresha miundombinu. 

Hospitali ya Rufaa ya Iringa inahudumia wakazi  zaidi ya milioni moja na nusu wa mkoa huo na Njombe pia ina uwezo wa kubeba vitanda 500 lakini vilivyopo ni 455. Kwa sasa inatoa huduma za kawaida na huduma zinazohitajika utaalamu zaidi kwa wagonjwa wanaopata rufaa kutoka hospitali za wilaya. Wastani wa wagonjwa wanaotibiwa kwa mwezi ni 4310 na wanaolazwa kwa siku ni 59.

Kukamilika kwa mradi huo ni jitihada kubwa iliyofanywa na Baba Askofu  wa jimbo katoliki la Iringa Mhashamu Tarciusius Ngalalekumtwa pamoja na baraza la maaskofu Tanzania (TEC) katika kuanzishwa kwa uhusiano wa Hospitali hizo mbili na kupendekeza kwa wafadhili kuwepo kwa mradi wa kuboresha huduma za Mama na mtoto  ambao ulipata fedha za utekelezaji. 

Mradi wa ujenzi wa wodi hiyo ya ghorofa moja lenye sehemu mbili za kulaza wagonjwa ulianza mwaka 2010 na kukamilika 2012  umegharimu shilingi bilioni moja milioni mia nane na arobaini na mbili ambazo zimetolewa na Hospitali ya a Vicenza  kwa upande  wa  ofisi ya Mkuu wa mkoa imechangia shilingi milioni 22 kwa ajili ya ujenzi wa mfumo wa maji taka na kujenga mfumo wa umwagiliaji kwa kutumia maji ya kisima.

No comments: