Tangazo

October 31, 2013

Wakurugenzi Watendaji wa Serikali za Mitaa Shinyanga watakiwa kusimamia miradi kwa umakini

RC Shinyanga, Ally Rufunga
Na Magdalena Nkulu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Shinyanga


Serikali Mkoani Shinyanga imetoa rai kwa watendaji wote hususani Wakurugenzi wa Mamlaka za serikali za mitaa kusimamia kazi za barabara kwa kufuata sheria na kanuni kinyume chake serikali haitasita kuchukua hatua kwa watendaji ambao watashindwa kusimamia miradi kwa umakini.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe.Ally N.Rufunga ametoa rai hiyo jana kwenye kikao cha Bodi ya Barabara kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Mhe.Rufunga amesema,usimamizi mbovu unaisababishia serikali gharama za matengenezo zisizo za lazima,hivyo kuathiri shughuli za miradi mingine ya maendeleo pamoja na kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara.

Amesisitiza watendaji kutumia wakandarasi wanaostahili kielimu na vifaa vya kutosha, kuepuka rushwa na Wakurugenzi wote na Katibu Tawala Mkoa,kufanya ukaguzi wa barabara ili kujiridhisha utekelezaji wake.

Amesema pia,wananchi wote wana jukumu la kuzilinda barabara na kuzitunza kwani ni muhimu katika shughuli za maendeleo kwa kusafirisha bidhaa mbalimbali na kushirikiana kuwabaini wanaohujumu miunndombinu hiyo ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.

Aidha,Mkuu wa Mkoa amemtaka Wakala wa barabara wa Mkoa kuwaelimisha watumiaji wa barabara matumizi ya alama mbalimbali za barabara na kufanyia matengenezo alama zilizoharibiwa.

Katika kikao hicho wajumbe wameazimia Mkoa uandae Kamusi ya mtandao wa Barabara unaoonesha barabara zote katika Mkoa wa Shinyanga wenye urefu wa Kilometa 5,126.22.

Vilevile mkoa unatarajia kujenga barabara moja yenye manufaa kiuchumi inayounganisha Mkoa wa Shinyanga na Mkoa wa Mwanza kupitia Halmashauri za Manispaa ya Shinyanga,Wilaya ya Shinyanga na Halmashauri ya Mji Kahama na Halmashauri ya wilaya ya Msalala ambapo upembuzi yakinifu umeshafanyika na itagharimu jumla ya Tshs.Bilioni 118.

Hoja nyingine muhimu iliyojadiliwa na wajumbe wa kikao hicho ni uzito wa mizigo ambao hauendani na uwezo wa barabara, ambapo wajumbe wametaka alama zinazoonesha uwezo wa barabara ili kudhibiti uzito wa mizigo inayozidi na inayoletea uharibifu wa barabara.

Meneja wa Wakala wa barabara Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Philipo Manenuka amesema sheria ya kuweka alama za kuonesha uzito wa barabara inatamka kuwa ni mamlaka yenyewe ya serikali za mitaa ndiyo inaamua.

No comments: