Tangazo

October 6, 2011

Chakula kupelekwa maeneo ya al-Shabab

Somalia
Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limeanza usambazaji mkubwa wa msaada kwa watu milioni moja katika maeneo yenye ukame nchini Somalia yanayodhibitiwa na wanamgambo wa kiislamu.

Shughuli za kusafirisha chakula kwa malori zitaendelea kutoka pwani kwenda maeneo yanayodhibitiwa na al-Shabab.

Shirika hilo limesema ni harakati kubwa kuwahi kufanyika na shirika hilo duniani kote.

Hatua hiyo imefanyika baada ya majadiliano mazito na al-Shabab, lililozuia mashirika mengi ya kutoa msaada ya kimagharibi kutoka maeneo yao miaka miwili iliyopita.

Umoja wa Mataifa umetangaza baa la njaa katika miji sita nchini Somalia- zaidi kwenye maeneo ya al-Shabab.

Maelfu ya watu wamekimbia kutafuta msaada wa chakula kwenye mji mkuu, Mogadishu, inayoongozwa na serikali dhaifu ya mpito, au kwenye makambi kwenye nchi jirani za Kenya na Ethiopia.

Mwezi uliopita, al-Shabab lilianza kuwaondosha watu kwenye makambi, yanayoendeshwa na mashirika ya ihsani katika maeneo ya wanamgambo hao, na kuwarejesha kwenye vijiji vyao.
Source: BBC Swahili

No comments: