Tangazo

March 15, 2013

AENDA JELA MIAKA 35 KWA KUSABABISHA VIFO VYA WANAFAMILIA SABA

NDUDU WA SAMSON DANIEL WALIOTEKETEA KWA MOTO 2010

Na Venance Matinya, Mbeya.

Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya imemhukumu kutumikia kifungo cha miaka 35 Samsoni Daniel Mwang’ombe baada ya kupatikana na hatia ya kuua bila kukusudia ndugu wa familia moja wapatao saba.

Akisoma mashtaka mbele ya Jaji wa mahakama hiyo, Samwel Karua, Mwendesha mashtaka wa Serikali Rhoda Ngole alisema mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Juni 21, 2010 kinyume cha kifungu cha 195 (16) kilichofanyiwa marekebisho Mwaka 2002.

Ngole aliiambia Mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo mwaka huo majira ya 2:00 hadi saa 2:30 usiku ambapo alifika nyumbani kwa baba yake akiwa na sigara mkononi huku akiivuta na baadaye kuidondosha sigara hiyo iliyosababisha moto kuwasha nyumba.

Aliwataja walioathirika na moto uliokuwa  umewashwa kutokana na sigara aliyokuwa ameidondosha mtuhumiwa  kuwa ni Daniel Mwang’ombe, Anitha Richard, Salome Mwang’ombe,Jane Samson, Diana Samson, Maria George na Cloud Samson.

Kutokana na kosa hilo, mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na kwamba aliua bila kukusudia ambapo alikiri kuwa akiwa anavuta sigara alidondosha kipande hicho ambacho kilikuwa bado kinawaka moto.

Aidha Mwendesha huyo aliiambia mahakama hiyo kuwa pamoja na mtuhumiwa kukiri kusababisha vifo bila kukusudia mahakama impe adhabu kali kwa mujibu wa sheria.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa  upande wa utetezi Sambwee Shitambala  alisema Mahakama inatakiwa kumwonea huruma na kumpunguzia adhabu mshtakiwa kutokana na yeye  kuwa miongoni mwa wafiwa.

Alisema mshtakiwa ameondokewa na wazazi, watoto na mke katika ajali hiyo ambapo hakuhudhuria mazishi yao pia amekaa muda mrefu akiwa  mahabusu ambapo amekaa kwa miaka mitatu na kuongeza kuwa mtuhumiwa ni kijana ambaye ni nguvu kazi ya taifa hivyo hastahili kufungwa.

Hata hivyo kutokana na utetezi huo Jaji Karua alisema kutokana na hali iliyojitokeza mtuhumiwa atatumikia kifungo cha miaka mitano kwa kila tukio ambalo ni kusababisha vifo saba hivyo jumla atatumikia miaka 35
Chanzo Mbeya Yetu Blog

No comments: